Acts 27:1-6

Paulo Asafiri Kwenda Rumi

1 aIlipoamuliwa kwamba tungesafiri kwa njia ya bahari kwenda Italia, Paulo na wafungwa wengine wakakabidhiwa kwa kiongozi mmoja wa askari aliyeitwa Juliasi, aliyekuwa wa Kikosi cha Walinzi wa Kaisari. 2 bTulipanda meli iliyotoka Adramitio, iliyokuwa inakaribia kusafiri kwenda kwenye bandari zilizopo pwani ya Asia, tukaanza safari yetu tukiwa pamoja na Aristarko, Mmakedonia kutoka Thesalonike.

3 cKesho yake tukatia nanga Sidoni, naye Juliasi akamfanyia wema Paulo, akamruhusu aende kwa rafiki zake ili wamtimizie mahitaji yake. 4 dKutoka huko tukaingia baharini tena na tukapita upande wa chini wa kisiwa cha Kipro kwa sababu upepo ulikuwa wa mbisho. 5 eBaada ya sisi kuvuka bahari iliyoko upande wa Kilikia na Pamfilia, tukafika Mira huko Likia. 6 fHuko yule kiongozi wa askari akapata meli ya Iskanderia ikielekea Italia, akatupandisha humo.
Copyright information for SwhKC